Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, August 24, 2010

KAMPUNI YA ZAIN YAFUTULISHA WATOTO YATIMA TANGA


Zain yafuturisha yatima Tanga

Kampuni ya simu za mkononi ya Zain kupitia mradi wake wa Build Our Nation, imetoa futari katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Orphanage Trust Team cha Tanga mjini kwa ajili ya mfungo wa Ramadhani.

Futari hiyo ambayo ilitolewa na Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain Tunu Kavishe iliambatana na misaada mingine kama vile vyandarua 90 pamoja na vyakula vikiwemo mchele, Unga, Sabuni na Mafuta ya kupikia vilivyotolewa za Zain pia.

Akiongea wakati wa hafla hiyo Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain Tunu Kavishe alisema kuwa Zain wameamua kutoa msaada huo kama sehemu yake ya kujali jamii kupitia mradi wake wa Build Our Nation.

“Siku ya leo, tumeamua kufuturu pamoja na watoto yatima wanaotunzwa na kituo cha watoto yatima cha Orphanage Trust Team kilichopo cha hapa Tanga, hii ni sehemu muhimu kwetu katika kusaidia Jamii na pia kama ishara ya mshikamano unaonyeshwa na Zain kwa jamii na wateja wake, haswa wakati wa kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani”, alisema Tunu Kavishe, Meneja Huduma za Jamii wa Zain.

Akizungumzia msaada huo, Msimamizi wa kituo cha Orphanage Trust Team, Sheikh Hassani Waziri, alisema kuwa wamefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Zain kwa ajili ya kuwakumbuka watoto yatima katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani.

“Tunawashukuru sana Zain kwa kuwakumbuka watoto hawa yatima katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na naomba msaada huu uwe endelevu ili watoto hawa nao wapate fursa ya kufurahia maisha yao”.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga mjini Dr. Ibrahimu Msengi ambaye aliyehudhuria hafla hiyo aliishukuru kampuni ya Zain kwa kuonyesha moyo wa kusaidia watoto yatima katika kituo hicho.

Kwa mujibu wa Kavishe, mikoa mingine ambayo kutafanyika hafla za kufuturisha kutoka zain ni Dar es Salaam, Pemba, Songea, na Mbeya, Morogoro, Tabora, Kigoma na Kagera.

Kavishe alisema kuwa zaidi ya miaka mitano, mbali na juhudi za kusaidia jamii kwa namna mbalimbali hapa nchini, hususan katika sekta ya elimu, kampuni ya simu ya Zain imejiwekea utaratibu wa kuwa inafuturisha wadau mbalimbali katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...