Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, December 26, 2010

Miss Tanzania atoa msaada kituo cha watoto yatima cha Msongola Orphanage Trust Fund

Vodacom Miss Tanzania Genevieve Emmanuel akimkabidhi ndoo ya mafuta ya kula Joyce Haule mmoja ya watoto yatima wanaolelewa katika kituo cha Msongola Orphanage Trust Fund kilichopo Mvuti wilayani Ilala jijini Dar es Salaam. Aidha kampuni hiyo kupitia kampeni yake ya ‘Share n Care’ pia ilikabidhi vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili katika hafla iliyofanyika wakati wa sikukuu ya Christmas.

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kusherehekea sikukuu ya Christmas mrembo wa Vodacom Miss Tanzania Genevieve Emmanuel ameitumia siku hiyo kwa kula pamoja na kutoa msaada wa vyakula kwa watoto yatima wa kituo cha Msongola Orphanage kilichopo Mvuti, Ilala jijini Dar es Salaam.

Akiambatana na warembo wengine akiwemo Alice Lushiku, Salma Mwakalukwa ambaye ni balozi wa utalii nchini na Anna Peter Genevieve aligawa mchele, maharagwe, sabuni, chumvi, sukari, unga, mafuta ya kula, maji vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya milioni 2/-.

Akizungumza baada ya kula chakula na kucheza na watoto hao, mrembo huyo wa Vodacom Miss Tanzania alimpongeza Mwenyekiti wa kituo hicho Chantal Bwami kwa kujitolea eneo lake kwa ajili ya kujenga na kuwalea watoto yatima takribani 30.

Genevieve alisema ingawa kuna baadhi ya watu wana uwezo mkubwa wa kifedha na kihali hawana moyo wa kumlea hata mtoto mmoja tofauti na Bwani ambaye amejitolea kuwalea, kuwasomesha kupitia misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali.

“Nimefurahi kwa jinsi watoto walivyotupokea hali inayoonesha wanajisikia faraja kama wapo kwa wazazi wao. Kutokana na hilo naahidi kurudi tena Msongola Orphanage ili kujitolea misaada mingine ikiwemo vifaa vya kusomea,” alisema mrembo huyo.

Akisoma risala kwa niaba ya wenzake, yatima Happiness Saimon anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Msongola alisema kituo chao licha ya kukabiliwa na matatizo mengi changamoto kubwa wanayoikabili ni ukosefu wa choo bora, eneo la kulia chakula na kituo kutokuwa na uzio jambo linalohatarisha usalama wao.

Kwa upande wake Bwani aliishukuru Vodacom Tanzania kupitia kwa Genevieve kutokana na kukipa kipaumbele kituo chao kilichopo kilometa 100 kutoka jijini hivyo kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa yatima hao ili waweze kufikia malengo yao kimaisha.

Aidha Mtaalamu wa masuala ya habari wa kampuni hiyo Matina Nkurlu alisema msaada walioutoa ni muendelezo wa kampeni yao ya ‘Share & Care’ iliyolenga kuzifikia jamii zenye mahitaji ili kuweza kusherehekea vema sikukuu ikiwemo Christmas na mwaka mpya 2011.

“Leo kupitia Vodacom Miss Tanzania tumekula chakula cha mchana na kukabidhi vyakula mbalimbali kwa watoto hawa ili nao wajisikie wapo ndani ya familia kama watoto wengine na si kama yatima, Tunaahidi kuendelea kukisaidia kituo hiki kuendana na mahitaji kama tunavyofanya sasa,” alisema Nkurlu.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...