Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, January 13, 2012

James Kibosho aziba pengo la Chaz Baba Twanga


Na Mwandishi Wetu
MPIGA ngoma nguli wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta', James Kibosho, amerithi mikoba ya aliyekuwa mwimbaji wa bendi hiyo, Charles Gabriel 'Chaz Baba' aliyetangaza kujiengua wiki hii na kuhamia Mashujaa Musica.
Mmoja wa wanamuziki galacha wa Twanga Pepeta, Khamis Kayumbu 'Amigolas' jana usiku wakati wa onesho la Twanga Pepeta kwenye ukumbi wa Club Bilicanas, alimtangaza Kibosho kuwa ndiye kiongozi wa kupanga muziki jukwaani (Stage Master), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Chaz Baba.
Tangazo hilo la Amigolas lilipokewa kwa hoi hoi, nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki kochokocho wa Twanga Pepeta waliojaa pomoni ukumbini hapo kushuhudia burudani ambayo pia ilishuhudiwa na mwimbaji wa bendi ya Mapacha Watatu, Kalala Hamza 'Junior', Meneja wake, Hamisi Dacorta na wanamuziki wengine wa FM Academia, Patcho Mwamba na Pablo Masai.
Waimbaji wa Twanga Pepeta, Ramadhan Athuman 'Dogo Rama', Venance Mgori na rapa na mwimbaji, Jumanne Said, wakiongozwa na kiongozi msaidizi wa bendi hiyo, Saleh Kupaza, walidhihirisha hakuna pengo lililoachwa na Chaz Baba kutokana na kuimba kwa ufasaha, 'vipande' alivyokuwa akiimba.
Wanamuziki wengine wa Twanga Pepeta waliokuwa jukwaani kuongoza mashambulizi ni kiongozi mkuu, Luiza Mbutu, Amigolas, Haji Ramadhan (mshindi wa BSS 2011), Mwinjuma Muumin, Janeth Isinika, Khadija Mnoga 'Kimobitel', Grayson Semsekwa na Msafiri Said 'Diouf'.
Pia walikuwepo wapiga vyombo, Miraji Shakashia 'Shakazulu', Jojoo Jumanne, Godfrey Kanuti, Selemani Shaibu, Victor Nkambi na Hassan Kado. Wanenguaji ni Asha Said 'Sharapova', Maria Soloma, Betty Johnson 'Baby Tall', Mary Khamis na wengineo.
Twanga Pepeta hivi sasa inatamba na albamu yake ya 11 ya Dunia Daraja yenye nyimbo za Kauli, Kiapo cha Mapenzi, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Dunia Daraja na Penzi la Shemeji.
Albamu zilizopita za bendi hiyo ni Kisa cha Mpemba (1999), Jirani (2000), Fainali Uzeeni (2001), Chuki Binafsi (2002), Ukubwa Jiwe (2003), Mtu Pesa (2004), Safari 2005 (2005), Password (2006), Mtaa wa Kwanza (2007) na Mwana Dar es Salaam (2009).

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...