Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 5, 2012

Elimu ya sanaa irudishwe tena mashuleni kuanzia shule za awali



Wanafunzi waliohitimu Alphabeta Music Centre, Tabata
Asilimia kubwa ya wanamuziki hapa Tanzania wanapiga muziki bila ya kuwa na elimu yoyote ya awali ya muziki. Viongozi wengi wa nchi wamekuwa wakitoa kauli nzuri za kusifu sanaa hii na wasanii wa sanaa hii lakini ni nadra kusikia kiongozi akiongelea matayarisho rasmi katika sanaa hii, na kwa ukweli hata katika sanaa nyingine.
Kama ambavyo kumekuweko na kufa kwa viwanda nchini humu ndivyo ilivyotokea katika elimu ya sanaa. Zamani sanaa ilianza kufundishwa kuanzia darasa la kwanza, na hata syllabus ya elimu hiyo mpaka leo ipo, ila haitumiki. Vyuo, kama Chuo cha Waalimu Butimba kule Mwanza, kilitoa waalimu ambao walikuwa maalumu kwa ajili ya kufundisha sanaa katika shule zetu kuanzia shule za msingi, bahati mbaya sana haya yote yametupwa uvunguni, hivyo Taifa linakwenda kihobelahobela katika tasnia ya sanaa. Kuna vyuo, kwa mfano Chuo cha Sanaa Bagamoyo, ambacho hupokea wanafunzi kwa ajili ya kupata elimu ya sanaa, lakini utaona wazi kwa kuwa hakuna mtiririko wa elimu hiyo kutokea shule za msingi, elimu hiyo ina walakini. Na zaidi katika ngazi ya Chuo Kikuu, mtu anapata digrii baada ya kusoma miaka mitatu  bila ya kuwa na elimu ya awali inayoonyesha mtu huyu alikuwa na vyeti gani vya msingi katika taaluma yake.
Utafiti umeonyesha kuwa kupata elimu ya muziki kuanzia umri mdogo kuna faida nyingi sana. Kwanza humuwezesha mtoto kukuza sehemu ya ubongo ambayo huhusika na lugha na pia kukuza uwezo wake wa kutafakari. Inaeleweka kuwa ubongo huendelea kupata maendeleo miaka mingi baada ya kuzaliwa, hivyo muziki huendeleza kuboresha upande wa kushoto wa ubongo ambao ndio huhusika na ujuzi wa lugha na  tafakari. Muziki husaidia sana watoto kukumbuka mambo mbalimbali, ndio maana hata matangazo ya biashara ya kawaida husindikizwa na muziki ili kukaa katika kumbukumbu kwa urahisi. Kwa watoto, muziki husaidia sana katika kazi zao za elimu ya kila siku.
Wasanii waliopata elimu sahihi huwa na uwezo wa kubuni majibu mbali mbali kwa tatizo moja, hii unaweza kuiona kwa mfano ukiwapa wanamuziki kumi semina kuhusu jambo, kwa mfano ukimwi kisha ukawambia watunge wimbo kuhusu elimu waliyopewa, utashangaa watakuja na tungo tofauti za mtizamo mpya kabisa wa kuelezea elimu hiyo waliyoipata. Elimu ya muziki  hufungua ubongo  kuruhusu kuachana na mawazo mengi yaliyopita na kujaribu mawazo mapya. Wasanii kote duniani huwa waanzilishi wa mambo mengi ikiwemo mitindo ya nguo, uvaaji na mambo mengi katika maisha kutokana na ubongo wao kuwa na uwezo wa kuruhusu kufikiria vitu katika mtazamo mpya. Elimu ya awali ya muziki imeonyesha kuwa wanafunzi wa elimu hii hufanya vizuri zaidi katika masomo mengine, tofauti sana na mawazo ya kawaida kuwa muziki huharibu watoto. Katika muziki, kosa huwa ni kosa , ukikosea beat, usipotyuni chombo chako, ukiimba vibaya ni kosa hakuna mbadala, sauti ikiwa juu mno, au chini mno nakadhalika, na mwananmuziki hulazimika kurudia tena na tena mpaka atakapopata kitu sahihi kabisa, elimu hii ikiwa kichwani kwa mtoto toka umri mdogo humsaidia katika kuboresha mambo yake mengine na kuyafanya vizuri zaidi kila mara. Elimu ya awali ya muziki humjenga mtoto kujua kufanya kazi na watu wengine kama kundi, kutokana na kuelewa kuwa katika muziki watu wengi hutegemeana ili kuleta ubora katika wimbo mmoja, hii huwasaidia katika maisha ya kila siku. Kuna mengi yanayopatikana katika elimu bora ya sanaa, pia kubwa likiwa ni kwenda sambamba kitaaluma na ulimwengu, kuna bahati mbaya sana kwa vijana wetu kutaka kuingia katika soko la muziki duniani lakini bila kuwa na matayarisho yanayostahili kufikia huko, wengi ndoto zao hazitatimia kwani elimu ya kufikia huko hawana.

2 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...