Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 5, 2012

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AMKARIBISHA BALOZI WA SUDAN NCHINI NA KUMUAGA WA MSUMBIJI, IKULU JUNI 05, 2012



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Sudan nchini Tanzania, Dkt. Yassir Mohammed Ali, wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam leo Juni 05, 2012 kwa mazungumzo. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo Jumanne ya Tarehe 05 Juni 2012 amekutana na Mabalozi wa nchi za Sudan na Msumbiji waliomtembelea ofisini kake Ikulu jijini Dar es Salaam.
 
Balozi wa kwanza kufika alikuwa Balozi wa Sudan nchini Tanzania Mheshimiwa Dkt. Yassir Mohamed Ali ambaye amekutana na Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza na katika kujitambulisha kwake akaelezea nafasi ya Tanzania katika kuhakikisha Bara la Afrika linabakia kuwa na amani na utulivu.
 
Balozi Mohammed alimwambia Makamu wa Rais kuwa wafanyabiashara kutoka Sudan wamekuwa wakishiriki katika uwekezaji nchini na bado wapo ambao wana nia ya kufanya hivyo na kwa kuanzia wafanyabiashara hao watashiriki katika maonyesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Saba Saba yatakayofanyika mwaka huu. Balozi huyo alieleza pia kuwa, Sudan inadumisha uhusiano wake na Tanzania katika kuhakikisha nchi mbili zinabakia kuwa na lengo moja kubwa la kuwapatia wananchi maendeleo.
 
Kwa upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais, yeye alimkaribisha Balozi Mohammed na kumwahidi kuwa Tanzania itazidi kutumia nafasi yake katika kuhamasisha amani hasa sasa ambapo nchi ya Sudan iko katika mgogoro na Sudan ya Kusini.
 
Balozi Amour Zacarias Kupela wa Msumbiji, yeye sambamba na kumuaga Mheshimiwa Makamu wa Rais alimwambia kuwa amefurahi sana kuwepo nchini Tanzania na kwamba anaithamini nchi hii kama nyumbani kutokana na uwezo wake wa kudumisha amani na pia kwa nafasi yake katika kuhakikisha wananchi wa Msumbiji wanakuwa huru na wanaishi kwa amani kama ilivyo sasa.
 
Balozi huyo alisema serikali ya Msumbiji inatumia fursa zake za kuhakikisha inakuza kilimo ili kutoa nafasi ya kuwepo chakula cha kutosha nchini humo na
pia akafafanua kuwa hali ya kisiasa nchini mwake kwa sasa ni shwari na hivyo wananchi wa ajukumu moja tu la kujitafutia maendeleo.
 
Balozi Maricias alifafanua kuwa upo umuhimu wa kukuza nafasi za kubadilishana wanafunzi kati ya Msumbiji na Tanzania kwani kama haitafanyika hivyo ni rahisi wananchi wa nchi hizi kusahau historia ya namna nchi hizi mbili zilivyoshirikiana katika kipindi cha kupigania uhuru.
 
Makamu wa Rais alimueleza Balozi Maricias kuwa, Tanzania inashukuru sana kwa mchango wake alioutoa kama Balozi na pia katika kazi alizofanya kabla ya kuwa Balozi. Alimtakia kila la kheri katika kazi zake mpya huku akimhakikishia kuwa Tanzania itabakia na mahusiano chanya na Msumbiji katika kipindi chote.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...