Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Sunday, June 10, 2012

Miss Kigamboni kufundwa kesho na Kamati ya Miss Tanzania


Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya urembo ya Miss Tanzania inatarajia kesho kukutana na warembo wanaowania taji la kitongoji cha Kigamboni 'Miss Kigamboni 2012' kwa ajili ya kuwapa 'darasa' na kufahamu taratibu na malengo ya shindano hilo.
Shindano la urembo la kitongoji cha Kigamboni linatarajiwa kufanyika Ijumaa ya Juni 15 kwenye Ukumbi wa Navy Beach kuanzia saa 1:00 usiku.
Akizungumza jana, Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu, alisema kuwa warembo hao pia watapata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na sanaa hiyo ambayo mshindi wake kitaifa hupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia.
Alisema kuwa maandalizi ya shindano hilo yanaendelea vizuri na mwaka huu kamati ya Miss Kigamboni imeamua kutoa sehemu ya fedha zitakazopatikana kwa lengo la kuipa heshima ya shule hiyo ambayo ni moja ya sehemu zilizotoa washiriki wa kinyang'anyiro hicho na wajumbe wa kamati ya maandalizi.
Alisema kuwa wanawaomba wakazi wa Kigamboni na wengine kutoka sehemu mbalimbali jijini kujitokeza kushuhudia warembo wao ambao hapo baadaye wataenda kukiwakilisha kitongoji hicho kwenye mashindano ya Kanda ya Temeke.
Aliitaja bendi muziki wa dansi ya FM maarufu kama 'Wazee wa Ngwasuma' pamoja na msanii wa vichekesho Mpoki ambaye ni mkazi wa Kigamboni watatoa burudani ya aina yake katika shindano hilo.
Aliwataja warembo wanaojiandaa kuwania taji hilo kuwa ni pamoja na Carolyne Dandu, Fatina Francis, Edda Slyvester, Aisha Mussa, Rosemary Peter, Doreen Kweka, Carolyne Peter, Agnes Goodluck, Sophia Martine, Rosemary Deogratius, Beatrice Boniface, Julieth Philip, Khadija Kombo na Winnie Karaya.
Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kudhamini shindano hilo ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF,Hope country Motel, Norbro’s Collections, Screen Masters, Clouds FM, Times FM na Global Publishers.
Warembo watakaofanya vizuri watachuana na wenzao wa Chang'ombe na Kurasini kuwania taji la Kanda ya Temeke hapo baadaye.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...