Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, June 19, 2012

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUTUMIA VEMA UTII WA SHERIA NA VIONGOZI



 
Na Christina Mponji wa Jeshi la Polisi.
 
Viongozi wa dini za Kikristo na Kiislam wametakiwa kutumia vema nyadhifa na fursa walizonazo katika kuhakikisha kuwa waamini wao wanatii sheria bila ya kushurutishwa.
 
Wito huo umetolewa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi wakati alipokuwa akizindua kampeni ya utii wa Sheria Bila Shuruti kwa viongozi wa dini za Kiislam na Kikristo.
 
Mhe. Mwinyi amewataka viongozi hao kutumia fursa wanazozipata kupitia Ibada na Swala katika kuwahubiria waamini wao kuhusiana na suala zima la kutii Sheria bila ya kushurutishwa.
 
Amesema kuwa kwa kuwa viongozi hao wa dini ndio watu pekee ambao wanakuwa na watu wote katika nyakati zote za maisha yao bila kujali itikadi wala kabila, hivyo ni rahisi kwao kuwashawishi waumini hao watii sheria bila ya kushurutishwa kutokana na imani waliyonayo juu yao.
 
Aliongeza kuwa endapo kila kiongozi atafanikiwa kuwashawishi waamini wake watii sheria bila ya kushurutishwa, nao wakatii , basi ni wazi kuwa uhalifu utapungua nchini na amani yetu itadumu daima.
 
Alhaji Mwinyi pia amewasifu viongozi hao wa dini kwa hatua waliyoichukua ya kuweza kukaa pamoja bila ya kujali itikadi zao na kufikia muafaka wa kuanzisha kampeni hiyo ambayo ina lengo la kudumisha amani nchini.
 
Mhe. Mwinyi alitoa rai kwa taasisi za Kiserikali, Sekta binafsi pamoja na mtu mmoja mmoja kuzingatia utii wa sheria bila ya  kushurutishwa kwa kufanya hivyo kutaleta tija kwa taifa.
 
“Watumishi wa Umma wakitii sheria bila ya kushurutishwa wananchi watapata huduma kutoka kwa watumishi hao vizuri na kwa hivyo itaondoa fikra potofu za kwamba watumishi wa Umma hawatekelezi wajibu wao mpaka kwa kusukumwa”
 
Aidha Alhaji Mwinyi amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kukabiliana na uhalifu nchini ikiwa ni pamoja na busara aliyoitumia katika kuwashawishi viongozi hao wa dini hata wakafikia kukaa pamoja na kuanzisha kampeni hiyo.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wenzake, Sheik Issa Othman Issa amewataka watanzania kupokea mafundisho mema yanayotolewa na viongozi wao wa dini ili kujenga taifa bora na lenye kutii mamlaka zilizopo.
 
Sambamba na uzinduzi huo pia kulizinduliwa vitabu vya ‘Utii wa Sheria ni Wajibu, kufuata sheria bila shuruti ni thawabu’ kilichoandaliwa na Taasisi ya Kiislamu ya Mwinyi Baraka na kitabu cha ‘Baraka za utii bila shuruti’ kilichotolewa na Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania.
 
Uzinduzi wa kampeni hiyo iliyokuwa na kauli mbiu ya’ Utii wa Sheria ni Thawabu’ kwa upande wa Kiislamu na ‘Baraka za Utii wa Sheria’  kwa upande wa Kikristo ulifanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee na kuhudhuriwa na viongozi wa dini zote mbili kutoka mikoa mbalimbali nchini.





No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...