Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, June 4, 2012

Wanakibasila wapinga fidia ya mabasi yaendayo kasi DART



Na Philemon Solomon wa Fullshangwe Dar es salaam
WAKAZI wa Kibasila Kata ya Gerezani ambao nyumba zao zilibomolewa kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo kasi wamepinga fidia inayotolewa na DART wakidai inapingana na sheria.
Akizungumza katika mkutano na wananchi hao Dar es Salaam juzi, Wakili  Dk. Edmund Mvungi kutoka Shirika la Wanasheria wa South Law Chambers alisema malipo hayo ni batili.
Alisema DART kwa siku kadhaa mfululizo imekuwa ikitoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuwa waliobomolewa waende kuchukua fedha za fidia.
Alisema DART walidai kuwa wakazi hao waliobomolewa nyumba hizo watalipwa donge nono la fidia ya sh.milioni 30 kufidia ardhi yao iliyotwaliwa na serikali.
Alisema sheria haielekezi hivyo fidia ya ardhi hutolewa baada ya bomoabomoa kwani fidia ni matokeo ya makubaliano kati ya serikali na wamiliki halali wa ardhi inayochukuliwa na kuwa sheria inaagiza kuwa kigezo ni bei ya soko.
Amesema DART kwa makusudi wameamua kukiuka sheria kwa kuanza kutangaza kufanyika kwa malipo hayo licha ya jambo hilo kuwa mahakamani.
Alisema fidia hiyo ni kinyume na sheria hivyo wao wamependekeza kila mmoja wao kulipwa sh. bilioni 2 kama fidia ardhi yao na usumbufu wa kubomolewa makazi yao.
Alidai wanakusudia kufungua kesi   mahakamani dhidi ya Mkurugenzi wa DART Kosmas Tekule kwa kukikuka sheria kwa kuanza kuwarubuni baadhi ya wananchi hao na kuanza kulipa fidia wakati suala hilo lipo mahakamani.
Katika hatua nyingine alisema wanakibasila hao hawawatambui wenzao 28 ambao wamerubuniwa kuchua fidia hiyo na kupitia kamati yao bandia ambapo walidai uongozi wanaoutambua ni ule unaosimamia kesi yao namba 44.
Viongozi hao wanaotambulika wametajwa kuwa ni Abdalla Mkongo, Jumbe Lilla, Hussein Batenga na Athman Kiwaga.
Alisema matangazo yanayotolewa na DART ni uchochezi na uvunjaji wa sheria kwani anayetoa matangazo hayo anaingilia kesi iliyopo mahakamani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...