Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Thursday, July 26, 2012

Hosptali ya AICC kuendesha kampeni ya kupima kisukari bure



Arusha, Tanzania.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kupitia hospitali yake ya AICC kitaendesha kampeni ya kupima kisukari bure kwa wakazi wa Arusha ili kusaidia wananchi kutambua kama wana ugonjwa wa kisukari au wapo katika hatari ya kuugua ugonjwa huo.

Kampeni hiyo itafanyika kesho (terehe 26-07-2012) katika hopitali ya AICC iliyopo jijini Arusha ambapo madaktari wa hospitali ya AICC kwa kushirikiana na madaktari wa wanaohudhuria mkutano wa Shirikisho la Madaktari wa Kimataifa pamoja na madaktari kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania wataendesha zoezi la upimaji huo.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Bwana Elishilia Kaaya, amesema kuwa mbali na kupima kisukari, madaktari hao pia watatoa ushauri wa namna bora ya kuishi na jinsi ya kuzuia madhara ya kisukari kwa wale watakao kuwa wamekutwa na ugonjwa huo.

 “Hospitali ya AICC inatambua umuhimu wa afya za wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla na ndio maana tumeona ni vema kufanya kampeni hii ya kupima kisukari. Napenda kutumia fursa hii kuwaalika wakazi wote wa Arusha na vitongoji nyake kufika kwa wingi kwani mbali na kupima pia itatolewa elimu na ushauri kutoka kwa wataalamu hao.” alieleza Kaaya.

Kwa mujibu Mkurugenzi Mwendeshaji, upimaji huo utaenda sambamba na mkutano wa kwanza wa Shirikisho la Madaktari wa Kisukari wa Kimataifa ambao kwa mara ya kwanza unafanyika hapa nchini. Mkutano huo utafanyika katika kituo cha AICC ambapo madaktari wanaohudhuria mkutano huo na wale kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania watatoa huduma ya upimaji katika zoezi hilo.

“Tunaamini baada ya kampeni hii wananchi watakuwa wamepata ufahamu juu ya hali ya afya zao na kutumia vema ushauri wa madaktari kwa ajili ya kujikinga na kuzua athari za ugonjwa huo”, alielezea Kaaya.

Mbali na kuendesha kampeni hii, hospitali ya AICC imeanzisha kitengo maalumu cha kisukari ambapo kila wiki madaktari hutoa huduma za matibabu na ushauri kwa wagonjwa wa kisukri.

Ugonjwa wa kisukari umekuwa ukiongezeka kwa kasi duniani ambapo taarifa za Shirika la Afrya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2011 watu milioni 366 walikuwa wanaugua ugonjwa wa kisukari na mwaka 2030 idadi inakadiriwa kufika milioni 552. Barani Afrika watu milioni 14 na nusu wanaugua ugonjwa huo huku idadi ikitarajiwa kufika milioni 28 mwaka 2030 ikiwa ni ongezeko la asilimia 90.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...