Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Friday, August 31, 2012

SIMBA, YANGA ZAKOMOANA USAJILI, ZAWEKEANA PINGAMIZI TFF



 Wachezaji wa Simba na Yanga wakisalimiana katika moja ya mechi baina yao

DAR ES SALAAM, Tanzania
WAKATI Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa ikitarajiwa kukutana kesho Jumapili Septemba 2 kupitia pingamizi za usajili kwa wachezaji msimu wa 2012/13, klabu ya Yanga imeiwekea Simba pingamizi mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kuwa, Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo.

“Pingamizi la Yanga kwa Simba kuhusu nyota hao ni kuwa, walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame wakiwa na Simba. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/13,” alisema Wambura.

Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa, imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa, kwa maelezo inao nyot wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano, ambapo imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.

Wakati yenyewe ikiweka pingamizi hizo kwa Simba, Yanga imewekewa pingamizi mbili Kagera Sugar inayopinga usajili wa beki David Charles Luhende kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa, huku Simba nayo ikipinga usajili wa Kelvin Yondani kwa madai ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23, 2011.

Kwa mujibu wa Wambura, jumla ya wachezaji 17 wamewekewa pingamizi za usajili wao kwa klabu za Ligi Kuu, ambapo Simba licha ya kupinga usajili wa Yondani, yenyewe inapingwa kuwasajili Edward Christopher Shija na Samir Said Luhava wa Falcon ya Chakechake, Pemba kwa madai ya kutofuatwa kwa taratibu za uhamisho wao

Azam FC kwa upande wake inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani, wakati Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga.

Katika madai yao hayo, Simba inasema Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1 mwaka huu mbele ya viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) klabu ya APR, akilipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.

Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili na Kagera Sugar na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao, huku Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy.

Rollingstone inataka kulipwa fidia ya kumlea Makassy aliyejiunga Simba akitokea Yanga, kwa kuwa mchezaji huyo bado hajafikisha umri wa miaka 23, kama taratibu za uhamisho na matunzo ya mchezaji zinavyoelekeza.

Aidha, Wambura aliongeza kuwa, Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.

ITC hiyo ilitumwa juzi Agosti 30, hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu, huku zikiwa zimesalia siku tatu kufungwa kwa dirisha la usajili wa wachezaji hapo Septemba 4.

Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba.

ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati wowote kwani tayari TFF limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...