Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Tuesday, September 25, 2012

Serikali yatoa Ufafanuzi kuhusu Operesheni Ondoa Wavamizi wa Ardhi huko Madale jijini Dar es Salaam


RC Dar, Saidi Mecki Sadiki
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.

Dar es salaam.

 Serikali imesema kuwa haitayavumilia makundi ya watu wanaovunja sheria za nchi kwa kuendesha vitendo vya wizi, uvunjaji wa nyumba, uporaji na uuzaji wa ardhi kinyume cha sheria katika maeneo yanayomilikiwa kihalali jijini Dar es salaam.

 Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam kufuatia vurugu zilizotokea katika eneo la Madale nje kidogo ya jiji la Dar es salaam kutokana na uamuzi wa serikali kuwaondoa kwa nguvu wananchi waliovamia maeneo hilo.

Amesema kuwa serikali haikukurupuka kuchukua hatua hiyo na kuongeza kuwa hatua zilizochukuliwa zimezingatia kanuni na taratibu za kisheria zikiwemo baraka za kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

“ Kufanyika kwa zoezi hili si kwamba serikali ya Kinondoni imekurupuka, hata kidogo haijafanya hivyo, zoezi hili limefuata kanuni na taratibu zote za kisheria ikiwemo uamuzi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es salaam na amri ya Mahakama”

Amefafanua kuwa matukio yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo hayo kwa baadhi ya makundi ya wananchi hasa vijana waliobeba silaha za jadi kuwashambulia, kuwajeruhi na kuharibu mali za wananchi wanaoishi katika eneo la  Madale kihalali kwa lengo la kuwaondoa kwa nguvu na kuyatwaa maeneo yao ni jambo lisilokubalika nchini.

 Amesema kuwa licha ya jambo hilo kuwa la muda mrefu na serikali kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kihalali wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa baadhi ya wananchi wamekuwa hawakubaliani na jambo hilo na hatimaye kuanza kuyavamia maeneo ya wazi ambayo mengine yanamilikiwa na taasisi na makampuni.

Ameongeza kuwa zoezi hilo la kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hayo lilizingatia taratibu zote ikiwemo hatua ya serikali kuwapa taarifa wahusika wote waliovamia maeneo hayo kuondoka wenyewe jambo ambalo hawakulifanya.

“Kabla ya kutumia nguvu kuwaondoa wananchi hao serikali iliwapatia taarifa ya kuwataka kuondoka wenyewe jambo ambalo walilikaidi na kuendelea kukalia maeneo hayo kinyume cha sheria.

“ Bado naendelea kusisitiza kuwa serikali ilifuata taratibu zote, kwanza tuliwashauri wamiliki halali kwenda mahakamani kisha mahakama ikatoa amri ya wavamizi hao kuondolewa na zaidi ya hapo walipewa taarifa ya kuondoka wao wenyewe jambo ambalo hawakulifanya na hii inaashria kudharau amri ya mahakama” amesisitiza Bw. Sadiki.

Aidha Bw. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa imebainika kuwa  baadhi ya wananchi wanaoendesha vitendo hivyo vya kihalifu sio raia wa Tanzania na kukongeza kuwa tayari vyombo vya dola vinavyohusika vinaendelea na uchunguzi wa  suala hilo na tayari vinawashikilia watu 68 kwa kuhusika na vurugu hizo.

Pia ameonyeshwa kusikitishwa na baadhi ya watendaji wachache wa serikali na viongozi wa siasa wanaoshabikia na kuhamasisha suala hilo na kuongeza kuwa serikali inaendelea na uchunguzi wa suala hilo na ikibainika hathua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Katika hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Dar es salaam amevipongeza vyombo mbalimbali vya habari vinavyoendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi na kuongeza kuwa hivi sasa wananchi wana uelewa mkubwa juu ya zoezi hilo na wako tayari kuhesabiwa.

“Navishukuru sana vyombo vya habari kwa kazi nzuri za uhamasishaji wa watu kushiriki katika Sensa ya watu na Makazi japo vipo vichache sana vinavyoendesha mijadala ya kuipinga”

Amesema maandalizi ya zoezi hilo kwa mkoa wa Dar es salaam yamekamilika licha ya kuwepo kwa  malalamiko na madai ya baadhi ya makarani wachache kutolipwa fedha za mafunzo jambo ambalo amesema mamlaka husika zinalifanyia kazi kwa kuhakikisha kuwa ukamilishaji wa uhakiki na uthibitisho wa majina yao unakamilika leo.

“Kwa upande wa jiji la Dar es salaam wengi wameshalipwa fedha zao na kwa  wale wachache ambao madai yao yanashughulikiwa nawahakikishia kuwa watalipwa kwa kuwa fedha yao ipo” amesisitiza.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...