Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Monday, November 26, 2012

Hospitali za serikali zaonywa kuuza damu




Na Peter Mwenda

HOSPITALI zote za Serikali zimeonywa kuacha tabia ya kuuza damu kwa hospitali binafsi wakati inatolewa bure kwa kila anayehitaji huduma hiyo nchini.

Ofisa Mwendeshaji wa Mpango wa Damu Salama Tanzania, Dkt. Abdu Juma aliyasema hayo wakati wa uchangiaji damu uliofanywa na waumini wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kushirikiana na Mpango wa Damu Salama Tanzania uliofanyika nchini kote jana.

Dkt. Juma alisema wamepata taarifa kuwa hospitali za Serikali za Mikoa zimekuwa zikiuza damnu kwa hospitali binafsi na kuonya kuwa watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

"Tunapeleka damu hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali ya Manispaa ya Ilala, Hospitali ya Manispaa ya Temeke lakini tunasikia damu hiyo inatolewa hapo kupelekwa hospitali za binafsi" alisema Dkt. Juma.

Alisema mwaka huu Mpango wa Damu Salama ulikusanya chupa 106,000 tu ambayo ni sawa na asilimia 76 ya lengo ambalo ni chupa 400,000 kwa mwaka.

Dkt. Juma aliwashauri wananchi kujitokeza kuchangia damu kwa hiari hasa kipindi hiki ambacho wachangiaji wakubwa ambao ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanakwenda likizo.

Alisema ili kuongeza makusanyo ya damu aliwaomba watanzania kujitokeza kuchangia kupitia kwenye kanda zao zilizoko katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Arusha, Mtwara, Lindi, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Kiongozi wa utoaji Damu wa Khoja Shia Ithnasheri,Aliabdu Mamdani alisema kambi ya utoaji damu ya Ashura ambayo hujitolea kila Novemba 24 ya mwaka kutoa damu kwa hiari mwaka huu wanatarajia kukusanya chupa 350-400 za damu.

"Nawaomba wanajumuiya wote wa Khoja Shia Ithnasheri wa mikoa ya Morogoro, Arusha, Mtwara, Lindi, Mwanza na Dar es Salaam kujitokeza kutoa damu kuokoa maisha ya watanzania wanayopotea kwakukosa damu hospitalini" alisema Mamdani.

Ofisa Mawasiliano wa Mpango wa Damu Salama Tanzania, Rajab Mwenda alisema taarifa ya idadi ya chupa za damu zilizokusanywa sioku ya Ushura na waumini wa Shia Ithnasher itatolewa baadaye.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...