Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, February 15, 2014

MTOTO WA MAREHEMU DK. MGIMWA ACHUKUA FOMU ZA KUGOMBEA UBUNGE KALENGA


Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka akimkabidho fomu za uteuzi, Mgombea wa CCM Jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa
MTOTO  wa aliyekuwa mbunge wa  jimbo la Kalenga marehemu Dr Wiliam Mgimwa Bw Godfrey Mgimwa achukua  fomu ya  kugombea ubunge jimbo la kalenga kwa shamla shamla kubwa   katika  mji  wa Iringa.

Pamoja na kuchukua  fomu  hiyo kwa msimamizi wa uchaguzi  jimbo la  kalenga pia aliponda mbinu  zinazotumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika kampeni zake na kuwa kwa  upande wake amejipanga  kushinda katika  uchaguzi huo.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kuchukua fomu za uteuzi  wa kuwania nafasi hiyo kwa msimamizi wa uchaguzi wa wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka.

Kwa mujibu wa Kisaka saa 10 jioni ya Februari 18 ndio itakuwa siku ya mwisho ya kurejesha fomu za uteuzi kwa wagombea wote, kampeni zitaanza Februari 19 hadi Machi 15 na uchaguzi huo mdogo wa utafanyika Machi 16. 

Kabla ya na baada ya kuchukua fomu hizo, Mgimwa aliyetokea ofisi za CCM Iringa Vijijini zilizopo mjini Iringa, alisindikizwa na maandamano makubwa ya wana CCM yaliyozunguka katikati ya mji wa Iringa.

“Ni chama kinachoongoza kwa matumizi mabaya ya fedha za umma; kampeni za vijiji helkopta, kampeni za udiwani helkopta, ubunge nao helkopta, kwanini wanatumia vibaya fedha wanazopata badala ya kuzitumia kusaidia kutatua kero za wananchi?” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu aliongeza kwa kusema kwamba sio rahisi kwa viongozi wa Chadema kuyajua matatizo ya wapiga kura wakiwa angani.

“Ukiwa angani unawezaje kujua kama wananchi wanahitaji mchango wa maji, madawati, vifaa vya afya, tofali, mabati na vingine vingi, sio rahisi na huenda wanatumia mbinu hiyo ili kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo,” alisema.

Alisema CCM inayajua matatizo ya wananchi inayoendelea kuyashughulikia kupitia Ilani yake ya uchaguzi na michango yao na wadau wengine wa maendeleo.

“Hatuhitaji chopa katika kampeni zetu; Chadema walitumia fedha nyingi kwenye kampeni zao za chaguzi ndogo za udiwani lakini matokeo yake wameyaona na yamedhihirisha chopa sio suluhu ya matatizo ya watu,” alisema.

Akizungumzia vipaumbele vyake, Mgimwa alisema muda uliobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 sio mkubwa lakini endepo atapewa ridhaa na wananchi wa jimbo hilo kuwa mbunge wao anavyo vipaumbele alivyojiwekea.

“Zipo baadhi ya ahadi zilizotolewa na Dk William Mgimwa ambazo hazikutekelezwa, hizo sitazizungumzia katika kampeni zangu nikiamini zitatekelezeka kupitia vipaumbele nilivyojiwekea endapo wananchi wa Kalenga watanipa ridhaa,” alisema.

Alivitaja vipaumbele vyake kuwa ni pamoja na kuboresha huduma ya elimu, afya, maji, elimu, miundombinu na mawasiliano.

Katika kuyashughulikia hayo yote nina imani yale yaliyoahidiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dk Mgimwa yatakuwa yanatekelezwa.

Huku akikataa kuweka hadharani mipango mikakati itakayotumiwa kwenye kampeni zake, alisema ana matarajio makubwa ya kushinda katika uchaguzi huo kwakuwa CCM inakubalika na watanzania walio wengi tofauti na inavyofikirika na vyama vya upinzani.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...