Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Wednesday, May 28, 2014

SHIRIKA LA POSTA KUTOA HUDUMA KATIKA VIWANGO VYA KIMATAIFA

IMG_6281(2)Meneja Masoko wa Shirika la Posta Tanzania Bw. David George akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es salaam kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na shirika hilo hadi sasa ikiwemo kuanza kutumika kwa anuani za makazi na Misimbo ya posta (Post code) inayolenga kuboresha huduma za shirika hilo,kulia ni Kaimu Meneja huduma za barua Bw.Jason Kalile.
(Picha na Idara ya Habari Maelezo)
Frank Mvungi- Maelezo
Shirika la Posta Tanzania linatarajia kuanza kutoa huduma zake kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa anuani za Makazi na Misimbo ya Posta kabla ya Mwisho wa Mwaka huu.
Hayo yamesemwa na  Meneja Masoko wa Shirika hilo Bw. David George wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Akifafanua David  amesema kuwa kwa kuzingatia mpango kazi wake shirika hilo limedhamiria kufikia mwakani nusu ya Mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani iwe imefikiwa na huduma ya anuani za Makazi na Msimbo wa posta.
Aidha David amesema kuwa huduma hiyo tayari imeanza kutolewa katika Mikoa ya Arusha  ambapo imehusisha kata 8, Dodoma kata 8, na Dar es salaam  hadi kufika June 2014 kata 27 zitakuwa zimefikiwa ambapo lengo kuu ni kuboresha huduma  na kufikisha barua pamoja na vifurushi katika makazi ya wateja kwa wakati.
Pia David alieleza kuwa Shirika hilo lina mpango kabambe wa kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji na utoaji huduma za Posta nchini ili kunufaika na fursa zinazoletwa na mabadiliko ya teknolojia,kuboresha huduma,kukidhi mahitaji ya soko na kukabiliana na ushindani.
Akifafanua Bw. David amesema lengo ni na kuongeza tija kwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa.
Shirika la Posta Tanzania linatekeleza mpango wa miaka 10 ( 2014-2023) unaozingatia juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dira ya maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Matokeo wakubwa sasa,sera ya posta 2003,Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUKUTA),Mpango wa kurasimisha rasilimali za biashara za wanyonge (MKURABITA),Mfuko wa Taifa wa anuani za Makazi na Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA.)

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...