Marquee

Pata habari za Jamii,Biashara,Burudani na michezo!!

tangazo

Saturday, April 16, 2016

SERIKALI YA KOREA YAGHARAMIA UJENZI WA HOSPITAL YA CHANIKA UTAKAO GHARIMU BILIONI 8.8 ZA KITANZANIA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (kulia) na Makamu wa Rais wa Shirika la Koica la nchini Korea Kusini, Taemyon Kwon, wakiweka tofali kwa pamoja kuashiria uweka wa jiwe la msingi la Hospitali ya Chanika iliyopo Manispaa ya Ilala, inayojengwa kwa ufadhili wa nchi hiyo Dar es Salaam jana. Ujenzi huo hadi kukamilika utagharimu sh. bilioni 8.8 za kitanzania.
.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Mr Isaya (kulia), Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victriana Ludovic na Meneja wa Mradi wa ujenzi wa Hospitali hiyo Mr Kim wakiweka jiwe la msingi la Hospitali hiyo.
Meneja wa Mradi huo, Mr Kim akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na ujumbe wake ramani ya majengo ya Hospitali hiyo.Na Dotto Mwaibale
Hutuba na taarifa ya mradi huo zilisomwa.
Balozi wa Korea nchini Geum-young Song (katikati), akizungumza katika hafla hiyo.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na balozi wa Korea nchini Geum-young Song wameweka jiwe la msingi la Hospitali ya Chanika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam ambapo itakapo kamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi 4000.

Akizungumza katika hafla ya kuweka jiwe hilo la msingi Chanika jijini Dar es Salaam jana, Makonda aliishukuru serikali ya Korea kwa msaada wa ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo itawasaidia wananchi wa Chanika na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana.

"Tunawashukuru hawa ndugu zetu wa Korea Kusini kwa msaada wa kutujengea Hospitali hii nawaombeni wananchi kuitunza ili kila mtakapokuwa mnafika kutibiwa tuwakumbuke wakorea" alisema Makonda.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victorina Ludovic alisema ujenzi wa Hospitali hiyo utasaidia kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi wapatao 398,882 kutoka maeneo ya Chanika, Msongola, Zingiziwa na Majohe hivyo kupunguza muda na gharama ambazo wananchi wamekuwa wakitumia kufuata huduma hizo umbali wa kilometa 30 kwenda hospitali ya Amana ya Rufaa.

Ludovic alisema ujenzi wa mradi huo hadi utakapokamilika utagharimu dola la milioni 4 sawa na sh.bilioni 8.8 za kitanzania.Balozi wa Korea nchini , Geum-young Song amesema wakorea hawafurahishwi wanapoona mama na mtoto wanapoteza maisha wakati wa kujifungua nchini Tanzania.

"Nchi yetu kupitia shirika la Koica imeamua kujitolea kujenga hospitali hii ili kuwasaidia wananchi wa Tanzania kupata huduma bora ya afya ya mama na mtoto wakati wa kujifungua kwani hatupendi kuona wanapoteza maisha wakati wa kujifungua" alisema Young Song.

Balozi huyo aliipongeza serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Korea katika shughuli mbalimbali jambo linaloimarisha uhusiano baina ya wananchi wa nchi hizo.

DART YAHIMIZWA KUELIMISHA WAKAZI WA DAR

ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kuanza, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Katika kipindi hiki cha majaribio, ambacho madereva wameanza kutumia barabara za BRT, hakikisheni mnatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu namna ya kuvuka barabara, kuzuia wenye bodaboda kutumia barabara hizo kuelezea na matumizi ya taa za barabarani kwa madereva wote,” amesema.
Ametoa agizo hilo jana usiku (Ijumaa, Aprili 15, 2016) wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu aliwataka watendaji wa wakuu wa taasisi wahakikishe wanapanua wigo na kutumia vyombo vya habari vingi kadri iwezekanavyo pamoja na mitandao ya kijamii katika kuelimisha raia juu ya zoezi hilo.
Akifafanua kuhusu hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema miundombinu kwa ajili ya mradi huo imekamilika na usafiri huo utaanza hivi karibuni.
Mhandisi huyo ametumia fursa huyo kutoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu ya barabara hizo kwa sababu imeigharimu Serikali fedha nyingi.
Naye Mrakibu wa Polisi (SP), John Shawa kutoka Makao Mkuu ya Trafiki alisema kuanzia kesho zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka litaanza hivyo amewaomba wananchi kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani.
"Kuanzia kesho linapoanza zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka ni vema watu wakatumia vizuri barabara hasa madereva wa bodaboda na madereva wengine watambue kuwa hawaruhusiwi kupita katika barabara hizo," alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAMOSI, APRILI 16, 2016.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...